Rais wa Sudan Kusini kuendelea kubakia madarakani hadi 2021
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46738-rais_wa_sudan_kusini_kuendelea_kubakia_madarakani_hadi_2021
Bunge la Sudan Kusini Alhamisi limepiga kura kurefusha muda wa rais Salva Kiir kubakia madarakani hadi mwaka 2021.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jul 12, 2018 23:40 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini kuendelea kubakia madarakani hadi 2021

Bunge la Sudan Kusini Alhamisi limepiga kura kurefusha muda wa rais Salva Kiir kubakia madarakani hadi mwaka 2021.

Spika wa Bunge la Sudan Kusini Anthony Lino Makana amesema bunge hilo lilipiga  kura  kurefusha  muda  wa  kubakia madarakani kwa  rais Salva Kiir kwa  muda  wa  miaka mitatu  zaidi na kusema hatua hiyo ni dharura ili kuzuia kuwepo pengo la madaraka nchini humo.

Sheria  hiyo itamruhusu Kiir kubakia madarakani  hadi  mwaka  2021 hata  wakati  akiwa  anajishughulisha  na  duru  ya  hivi  karibuni kabisa  ya  majadiliano  ya  kimkoa  ya  amani  pamoja  na  makamu wake  wa  zamani  ambaye  hivi  sasa  ni  kiongozi  wa  waasi  Riek Machar katika  kumaliza  vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe  vya miaka  minne  sasa.

Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar

Uchaguzi ulikuwa  ufanyike mwaka  huu, lakini  mzozo  umesababisha muda  wa  kufanyika  uchaguzi  huo  kushindikana. Waziri  wa  sheria Paulino Wanawilla , ambaye  aliwasilisha  mswada  huo, alisema utazuwia serikali  kutangazwa  kuwa si  halali, wakati  muda  wake wa  kuwapo  madarakani  utakapomalizika.

Makumi ya maelfu ya wananchi wameshauwa na karibu milioni nne wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mapigano yaliyozuka Sudan Kusini mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua.