Shirika la Msalaba Mwekunduu latahadharisha kuhusu mgogoro wa wakimbizi Ethiopia
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetahadharisha kuhusiana na mgogoro wa wakimbizi nchini Ethiopia kufuatia machafuko ya hivi karibuni kusini mwa nchi hiyo.
Taarifa ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu imeeleza kuwa, wakimbizi wa machafuko ya hivi karibuni nchini Ethiopia wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kutokuwa na chakula, sehemu za kujihifadhi na huduma nyingine za awali na za kimsingi.
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema kuwa, endapo jamii ya kimataifa itaghafilika na kutoushughulikia mgogoro wa wakimbizi hao haraka iwezekanavyo basi huenda katika siku za usoni kukashuhudiwa hali mbaya zaidi.
Shirika hilo limetoa wito wa kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia hao wa Ethiopia walioyakimbia makazi yao baada ya kuibuka machafuko.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, limesema, zaidi ya wakimbizi wa ndani 800,000 nchini Ethiopia wanaishi bila makazi ya kutosha na kutokuwa na huduma muhimu na hivyo kusababisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu inayochochewa na baridi kali pamoja na mvua.
Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, machafuko yaliyolikumba eneo la kusini mwa Ethiopia tangu mwezi Juni mwaka huu ndiyo yaliyosababisha watu zaidi ya laki nane kuyahama makazi yao huku raia hao hivi sasa wakihitaji chakula na misaada mingine kwa ajili ya kujikimu kimaisha.