EU yafungua ubalozi wake wa Libya uliofungwa 2014
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46789-eu_yafungua_ubalozi_wake_wa_libya_uliofungwa_2014
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ameitembelea Tripoli, mji mkuu wa Libya na kufungua upya ubalozi wa umoja huo uliohamishiwa Tunis, mji mkuu wa Tunisia mwaka 2014.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2018 02:37 UTC
  • EU yafungua ubalozi wake wa Libya uliofungwa 2014

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ameitembelea Tripoli, mji mkuu wa Libya na kufungua upya ubalozi wa umoja huo uliohamishiwa Tunis, mji mkuu wa Tunisia mwaka 2014.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya jana Jumamosi imesema kuwa, "kurejea kwa ofisi ya kidiplomasia ya EU nchini Libya kutaimarisha ushirikiano kati ya umoja huu, serikali kuu na serikali za mitaa za Libya na Umoja wa Mataifa."

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekutana na kufanya mazungumzo na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali hiyo, Mohamed al-Taher Siala na Mjumbe Maalumu wa UN nchini Libya, Ghassan Salame.

Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayotambuliwa na UN

Baada ya kufanya kikao na maafisa hao, Federica Mogherini amesema, "Uwepo wetu Libya sasa utakuwa mpana zaidi, nimekuwa na mazungumzo ya kufana na al-Sarraj, na tukajadiliana kuhusu uungaji mkono wa EU kwa serikali na watu wa Libya. Tutaendelea kushirikiana na taifa hili katika masuala ya misaada ya kibinadamu, maendeleo, kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kubwa zaidi, uungaji mkono wa EU kwa mchakato wa kisiasa wa kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, hususan maandalizi ya uchaguzi."

EU ilifunga ubalozi wake mjini Tripoli na kuuhamishia mjini Tunis mwaka 2014, baada ya kushtadi ghasia na vuguvugu la mapinduzi lililoanza mwaka 2011, na kupelekea kung'olewa madarakani na kuuawa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.