Janga la mafuriko laua makumi ya watu Nigeria
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Nigeria yameua watu zaidi ya 49, na wengine 20 bado hawajulikano waliko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Niger.
Ripoti kutoka Nigeria zinasema kuwa, makumi ya nyumba zimebomolewa na kusombwa na maji kufuatia janga hilo la mafuriko huku mifugo wasiopungua 260 wakiwemo ng'ombe. mbuzi na kondoo wakiangamizwa.
Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo amesema kuwa, serikali itafanya kila iwezako kuhakikisha kuwa, waathirika wa mafuriko hao wanapatiwa misaada ya haraka.
Aminu Waziri, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Dharura katika Jimbo la Katsina amewaambia waandishi wa habari kwamba, hadi sasa miili ya wahanga 49 waliopoteza maisha katika janga hilo la mafuriko imepatikana.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Dharura amesema kuwa, kuna makumi ya watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo.
Kwa mujibu wa ripoti rasmi za serikali, maelfu ya watu wamebaki bila makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.
Nigeria iliyoko magharibi mwa bara la Afrika ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na mafuriko karibu kila mwaka ambapo mvua kubwa hunyesha nchini humo baina ya mwezi Mei na Septemba.
Mwaka 2012 Nigeria ilikumbwa na mafuriko makubwa katika majimbo 30 kati ya 36 ya nchi hiyo. Mamia ya watu waliaga dunia na wengine milioni mbili kuachwa bila makazi.