Afrika Kusini: Nchi zinazoizingira Qatar zinatushinikiza kuitenga nchi hiyo
(last modified Thu, 19 Jul 2018 07:45:42 GMT )
Jul 19, 2018 07:45 UTC
  • Afrika Kusini: Nchi zinazoizingira Qatar zinatushinikiza kuitenga nchi hiyo

Balozi wa Afrika Kusini nchini Qatar, amesema kuwa nchi yake inakabiliwa na mashinikizo ya nchi zinazoizingira Qatar kwa lengo la kukata uhusiano na nchi hiyo.

Faizel Moosa, aliyasema hayo akibainisha mwendelezo wa mashinikizo ya nchi zinazoizingira Qatar kuilenga Afrika Kusini na kusisitiza kwamba, siasa za nje za serikali ya Pretoria zimejengeka katika msingi wa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Balozi wa Afrika Kusini mjini Doha, mji mkuu wa Qatar amefafanua kwamba nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, hazitaki kuzungumza kwa ajili ya kuhitimisha migogoro inayozikabili na kwamba hakuna ratiba kwa ajili ya suala hilo.

Mgogoro kati ya Saudia na Qatar

Tangu tarehe tano Juni mwaka jana, nchi nne za Kiarabu marafiki wa Marekani, yaani Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri, zilitangaza kukata uhusiano wao na nchi ya Qatar ambayo nayo ni mmoja wa washirika wakubwa wa Marekani. Nchi nne hizo zilidai kwamba Qatar inayaunga mkono makundi tofauti ya kigaidi, sambamba na kuizingira kuanzia angani, baharini na ardhini. Hivi karibuni gazeti la Foreign Policy liliandika kuwa, licha ya kupita mwaka mmoja tangu kuibuke mzozo kati ya nchi hizo, hakujashuhudiwa matumaini yoyote ya kutatuliwa mgogoro huo.

Tags