Mahasimu Sudan Kusini wahindwa kufikia maufaka kuhusu kugawana madaraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46903-mahasimu_sudan_kusini_wahindwa_kufikia_maufaka_kuhusu_kugawana_madaraka
Utiwaji saini muafaka wa awali wa amani kati ya rais wa Sudan Kusini na mpinzani wake Riek Machar umeahirishwa, baada ya mahasimu hao kushindwa kuafikiana kuhusu namna ya kugawana madaraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2018 09:37 UTC
  • Mahasimu Sudan Kusini wahindwa kufikia maufaka kuhusu kugawana madaraka

Utiwaji saini muafaka wa awali wa amani kati ya rais wa Sudan Kusini na mpinzani wake Riek Machar umeahirishwa, baada ya mahasimu hao kushindwa kuafikiana kuhusu namna ya kugawana madaraka.

Ilitarajiwa kuwa, mkataba huo ungetiwa saini jana jijini Khartoum nchini Sudan na baadaye makubaliano rasmi kutiwa saini tarehe 26 mwezi huu.

Ripoti zinasema kuwa, serikali ya Sudan Kusini ndio iliyokataa  kusaini muafaka huo wa awali  baada ya Rais Salva Kiir, kuonekana kutokuwa tayari kuwa na makamu watano wa rais.

Nchi jirani ya Sudan imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya wawakilishi wa viongozi hao na wiki hii, walikubaliana namna ya kugawana madaraka.

Pande hasimu Sudan Kusini zimeafiki kugawana madaraka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo ambapo kwa mujibu wake kiongozi wa waasi nchini humo, Riek Machar atarejeshwa katika wadhifa wa Makamu wa Rais.

Itakumbukwa kuwa mrengo wa upinzani nchini Sudan Kusini na serikali ya nchi hiyo walifikia makubaliano katika juhudi za kuhitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Vita hivyo vilianza mwaka 2013 baada ya hitilafu za kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Machar kusababisha machafuko ya ndani.

Kutoka kushoto Rike Machar, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Omar el Bashir wa Sudan na Rais Salva Kiir Mayardit wakati wa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini mjini Khartoum hivi karibuni

Pande mbili hizo hasimu nchini Sudan Kusini zimehusika katika mauaji ya ulipizaji kisasi ambayo yaliibua miganyiko ya kikabila. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kufuatia machafuko hayo.

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini ambavyo vinaendelea tokea mwaka 2013 vimepelekea kuuawa kwa makumi ya maelfu ya watu wa nchi hiyo pamoja na wengine milioni nne kufanywa kuwa wakimbizi. Miezi kadhaa iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba ukame na njaa vinatishia maisha ya zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vimefanya shughuli ya kufikishiwa misaada ya chakula na kibinadamu, watu wanaoishi katika maeneo ya vita kuwa ngumu mno. Baada ya kufanyika kura ya maoni mwaka 2011, Sudan Kusini ilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake.