Ethiopia yatoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa
Ethiopia imepitisha sheria ambayo inatoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa ambao wameachiliwa hivi karibuni na kwa msingi huo kufuta sera ya miongo kadhaa ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani.
Sheria hiyo ni katika fremu ya marekebisho ya haraka ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanashuhudiwa Ethiopia tokea Waziri Mkuu Abiy Ahmed aingie madarakani mwezi Aprili. Marekebisho hayo yamejumuisha pia kurejeshwa uhusiano na nchi jirani ya Eritrea.
Serikali iliyotangulia ya Hailemariam Desalegn iliwakamata na kuwafunga jela karibu watu 30,000 kwa tuhuma za ugaidi kama njia ya kukabiliana na maandamano. Kati ya waliofungwa jela walikuwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, viongozi wa upinzani, waandishi habari na wanabologu.
Aidha maafisa wa usalama wanaripotiwa kuua mamia katika oparesheni za kukandamiza waandamanaji waliokuwa wakilalamikia utawala mbovu, udhalimu na ukandamizaji.

Abiy amekosoa vikali ukandamizaji na ukatili wa vikosi vya usalama na kuulinganisha na ugaidi wa kiserikali. Taarifa zinasema maelfu ya wafungwa wameachiliwa huru tokea mwezi Aprili kufuatia amri ya waziri mkuu huyo.
Bunge pia limepasisha sheria na kusema makundi yanayopigania kujitenga ya Oromo Liberation Front na Ogaden National Liberation Front pamoja na kundi la upinzani lililo uhamishoni la Ginbot 7 si makundi ya kigaidi.