Ethiopia kukumbatia demokrasia ya vyama vingi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46953-ethiopia_kukumbatia_demokrasia_ya_vyama_vingi
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema wakati umefika kwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iruhusu demokrasia ya vyama vingi ambayo msingi wake ni taasisi thabiti zinazoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2018 23:33 UTC
  • Ethiopia kukumbatia demokrasia ya vyama vingi

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema wakati umefika kwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iruhusu demokrasia ya vyama vingi ambayo msingi wake ni taasisi thabiti zinazoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Fitsum Arega, Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza habari hiyo katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Kutokana na uhalisia wa hali ya kisiasa hapa nchini hivi sasa, hakuna chaguo jingine ghairi ya kufuata mkondo wa demokrasia ya vyama vingi."

Amesema hilo litasaidia kusuluhisha tofauti zilizopo kwa njia za amani na kulihakikishia taifa maendeleo-endelevu.

Muungano tawala wa Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) umekuwa madarakani tangu mwaka 1991 na umekuwa ukidhibiti viti vingi bungeni.

Hailemariam Desalegn, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia

Ethiopia hivi karibuni ilipitisha sheria ambayo inatoa msamaha kwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa ambao wameachiliwa huru hivi karibuni na kwa msingi huo kufuta sera ya miongo kadhaa ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani, katika fremu ya marekebisho ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanashuhudiwa Ethiopia tokea Waziri Mkuu Abiy Ahmed aingie madarakani mwezi Aprili.

Serikali iliyotangulia ya Hailemariam Desalegn iliwakamata na kuwafunga jela karibu watu 30,000 kwa tuhuma za ugaidi kama njia ya kukabiliana na maandamano ya wapinzani na wakosoaji.