Mwanachuo aliyenyimwa cheti Nigeria kutokana na hijabu apata faraja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46989-mwanachuo_aliyenyimwa_cheti_nigeria_kutokana_na_hijabu_apata_faraja
Mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu aliyezuiwa mwaka jana kushiriki sherehe za mahafali kutokana na kuvaa vazi la hijabu mbali na kunyimwa cheti chake licha ya kupasi kwa Digrii ya Daraja ya Kwanza ya Juu katika somo la sheria, hatimaye amepata faraja baada ya mashinikizo kutoka kona mbalimbali hususan kwenye mitandao ya kijamii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2018 11:44 UTC
  • Mwanachuo aliyenyimwa cheti Nigeria kutokana na hijabu apata faraja

Mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu aliyezuiwa mwaka jana kushiriki sherehe za mahafali kutokana na kuvaa vazi la hijabu mbali na kunyimwa cheti chake licha ya kupasi kwa Digrii ya Daraja ya Kwanza ya Juu katika somo la sheria, hatimaye amepata faraja baada ya mashinikizo kutoka kona mbalimbali hususan kwenye mitandao ya kijamii.

Novemba mwaka jana, Chuo Kikuu cha Ilorin kilichoko katika jimbo la Kwara, magharibi mwa nchi, kilimpiga marufuku mwanachuo huyo wa Kiislamu kwa jina Amasa Firdaus Abdulsalam kushiriki sherehe za kuwatunuku wanachuo vyeti vyao na kuwaidhinisha rasmi kuwa mawakili, baada ya kukataa mwito wa kushiriki hafla hizo bila vazi la stara la hijabu.  

Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakilalamikia sheria za baadhi ya majimbo ya nchi hiyo za kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule binafsi hasa katika maeneo ambayo wakazi wake wengi ni Wakristo.

Wanawake Waislamu nchini Nigeria

Ikumbukwe kuwa, mapema mwezi Februari mwaka jana, Mahakama ya Rufaa katika jimbo la Lagos nchini Nigeria ilitoa hukumu ya kubatilisha amri ya serikali ya jimbo hilo ya kupiga marufuku vazi la hijabu kuvaliwa na wasichana Waislamu shuleni.

Hii ni katika hali ambayo, karibu asilimia 50 ya wananchi milioni 196 wa Nigeria ni Waislamu, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.