MSF yasimamisha shughuli zake Sudan Kusini baada ya ofisi zake kuvamiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46998-msf_yasimamisha_shughuli_zake_sudan_kusini_baada_ya_ofisi_zake_kuvamiwa
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imetangaza habari ya kusimamisha aghalabu ya huduma zake katika kaunti ya Maban, kaskazini mwa Sudan Kusini baada ya ofisi zake kushambuliwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2018 20:50 UTC
  • MSF yasimamisha shughuli zake Sudan Kusini baada ya ofisi zake kuvamiwa

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imetangaza habari ya kusimamisha aghalabu ya huduma zake katika kaunti ya Maban, kaskazini mwa Sudan Kusini baada ya ofisi zake kushambuliwa.

Samuel Theodore, mkuu wa jumuiya hiyo nchini Sudan Kusini amesema ofisi zao zilishambuliwa na watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha, ambapo mbali na kuiba vitu kadhaa vya shirika hilo, walichoma moto hema lililokuwa na vyombo vya matibabu na mawasiliano.

Amesema, "Na kwa kuwa usalama wa wafanyakazi wetu na vyombo vyetu hauwezi kudhaminiwa, hatuna budi kusimamisha sehemu kubwa ya huduma zetu, ingawaje watu zaidi ya 88,000 wataathiriwa." 

Jumuiya ya MSF inaendesha hospitali katika kambi ya wakimbizi ya Doro, sambamba na kutoa ushauri kwa hospitali ya serikali katika mji wa Bunj, makao makuu ya eneo la Maban kaskazini mwa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Mahasimu wa kisiasa wa Sudan Kusini baada ya kuafikiana kusitisha mapigano

Haya yanajiri huku mahasimu wa kisiasa nchini humo, Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani, Riek Machar wakitazamiwa kusaini rasmi makubaliano ya usishaji vita na kugawana madaraka kesho Alkhamisi.

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini ambavyo vinaendelea tokea mwaka 2013 vimepelekea kuuawa kwa makumi ya maelfu ya watu wa nchi hiyo pamoja na wengine milioni nne kufanywa kuwa wakimbizi.