Mapatano ya awali ya kugawana madaraka yafikiwa Sudan Kusini
Mahasimu nchini Sudan Kusini, Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar Jumatano walitilaina saini mapatano ya awali ya kugawana madaraka.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyofikiwa na viongozi hao mjini Khartoum, Sudan, Machar atarejesehwa nafasi yake ya makamu wa Rais. Akizungumza na waaandishi habari katika sherehe za kutiwa saini mapatano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Al-Dierdiry Ahmed amesema Kiir atanedelea kuwa Rais wa Sudan Kusini na Machar atakuwa makamu kwa kwanza wa rais. Ameongeza kuwa kutakiwa na makamu wengine wa rais ili kujumuisha makundi yote ya kisiasa katika madaraka.
Pande hasimu tayari zimeshatia saini mapatano ya kudumu ya usitishaji vita sambamba na kuondoa askari wao katika maeneo ya raia. Kwa mujibu wa mapatano hayo ya Jumatano kutakuwa na mawaziri 35 katika serikali ya mpito ambapo 20 watatoka kambi ya Kiir, 9 kutoka kambi ya Machar na waliosalia kutoka makundi mengine.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono na asilimia 99 ya raia wake baada ya vita vya miongo kadhaa vya kutaka uhuru. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.
Vita vya ndani nchini humo vilivanza Disemba 2013 na vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.