ICG: Mapigano baina ya wakulima na wafugaji Nigeria hatari kushinda Boko Haram
Shirika moja lisilo la kiserikali nchini Nigeria limesema watu waliouawa katika mapigano baina ya wakulima na wafugaji nchini humo ni mara sita zaidi ikilinganishwa na watu waliouwa katika hujuma za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2018.
Ripoti mpya ya asasi hiyo inayoitwa International Crisis Group (ICG) imebainisha kuwa, watu waliouawa katika mapigano hayo ambayo yanaelekea zaidi kuwa ya kikabila kati ya Januari na Juni mwaka huu ni zaidi ya 1,300.
Ripoti ya asasi hiyo imenukuu takwimu za Umoja wa Mataifa zinazoonesha kuwa, katika kipindi hicho cha miezi ya kwanza ya mwaka huu, watu 200 wameuawa katika mashambulizi ya kundi la ukufurishaji la Boko Haram.
Asasi hiyo ya kiraia imesema kuwa, changamoto hizo za kiusalama zinazoikabili nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na zinazotishia usalama na amani ya nchi hiyo, zitakuwa na taathira ya moja kwa moja katika uchaguzi mkuu wa Februari mwakani.
Mbali na mauaji hayo ya kikabila, serikali ya Rais Muhammadu Buhari inakabiliwa na zimwi la kundi la kigaidi la Boko Haram, lililoanzisha mashambulizi yake mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria.
Zaidi ya watu elfu 20 wa nchi hiyo na nchi jirani wameuawa katika hujuma hizo, huku wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita wakilazimika kuwa wakimbizi.