Amnesty International: Serikali ya Nigeria imeshindwa kudhamini usalama wa jimbo la Zamfara
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kwamba serikali ya Nigeria imeshindwa kudhamini usalama wa jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, kutokana na jimbo hilo kudhibitiwa na makundi ya wabeba silaha.
Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema kuwa utekaji nyara watu kila siku na hujuma zilizoongezeka za wabeba silaha katika maeneo yote ya jimbo hilo, vimewasababishia wasi wasi endelevu wakazi wake, kama ambavyo pia mapigano ya kikabila yanayojiri jimboni hapo yawamewafanya maelfu ya watu kuwa wakimbizi. Kwa mujibu wa Amnesty International, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, makundi ya wabeba silaha katika jimbo la Zamfara, yameua kwa akali watu 371.
Limeongeza kwamba, viongozi wa Nigeria na kwa mara kadhaa wamekuwa wakidai kwamba, wanafanya juhudi zenye lengo la kutatua mgogoro wa jimbo hilo, lakini takwimu za watu waliouawa katika mapigano na mashambulizi ya watu wenye silaha jimboni hapo, vinabainisha kwamba, serikali ya nchi hiyo imeshindwa kudhamini usalama wa eneo. Hii ni katika hali ambayo kufuatia ongezeko la mauaji jimboni hapo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, alitoa amri ya kutumwa maelfu ya askari katika jimbo hilo, hatua ambayo imetajwa na Amnesty International kuwa iliyofeli.