Kiir: Makubaliano mapya ya amani hayatasambaratika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47215-kiir_makubaliano_mapya_ya_amani_hayatasambaratika
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema anaamini kuwa makubaliano mapya ya amani baina ya serikali yake na kundi kubwa zaidi la waasi nchini humo hayatasambaratika kwa sababu sio ya kutwishwa kama yale ya kabla yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2018 20:57 UTC
  • Kiir: Makubaliano mapya ya amani hayatasambaratika

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema anaamini kuwa makubaliano mapya ya amani baina ya serikali yake na kundi kubwa zaidi la waasi nchini humo hayatasambaratika kwa sababu sio ya kutwishwa kama yale ya kabla yake.

Salva Kiir ambaye alikuwa akizungumza na waandishi habari mjini Juba amesema kuwa, atasafiri kwenda Khartoum huko Sudan kwa ajili ya kutia saini makubaliano ya amani na kundi la waasi la SPLM-IO linaloongozwa na mpinzani wake, Riek Machar. Sherehe ya kutiwa saini makubaliano hayo itafanyika kesho Jumapili.

Kiir amesema: "Makubaliano ya amani ya mwaka 2015 yalikuwa ya kutwishwa na kulazimishwa na hatukupewa fursa ya kuelea matakwa yetu".

Ameongeza kuwa mazungumzo juu ya makubaliano ya amani yamekamilika na matatizo yoyote na mpinzani wake yatatatuliwa baada ya kutiwa saini.

Kiir na hasimu wake, Riek Machar

Matamshi ya Kiir yametolewa baada ya makundi badogo madogo kueleza wasiwasi kwamba makubaliano ya sasa ya amani baina ya mahasimu hao wawili yatakuwa na hatima ile ile ya yale yaliyotangulia kutokana na kutoainishwa nafasi za kila upande katika ngazi zote za uongozi wa serikali ya Sudan Kusini.

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.