Aug 04, 2018 15:51 UTC
  • Upinzani, fujo na machafuko yaendelea baada ya uchaguzi nchini Zimbabwe.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe ameyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais akisema ni ya "uongo".

Nelson Chamisa ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba: fedheha iliyopata tume ya uchaguzi ambayo imetangaza matokeo ya uongo inasikitisha.

Chamisa ameongeza kuwa tume hiyo haikuruhusu chama chake cha MDC kipate taarifa za matokeo ya uchaguzi kabla ya kumtangaza Emmerson Mnangagwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Nkululeko Sibanda, afisa mwandamizi wa chama cha upinzani cha MDC amesema, watu 20 waliokamatwa na kupandishwa kizimbani wanakabiliwa na shtaka la kuwachochea watu kufanya fujo. Sibanda ameyasema hayo leo wakati kesi ya watu hao ilipokuwa inasikilizwa na kuongeza kuwa watu hao ni wafuasi wa chama chao cha MDC.

Rais Emmerson Mnangagwa (kushoto) na Nelson Chamisa

Mbali na kukosoa hali inayoendelea hivi sasa nchini Zimbabwe, kiongozi huyo wa MDC ameongeza kuwa watu wengi wamejificha kwa hofu na hali inayotawala nchini humo ni ya kutisha zaidi kuliko enzi za Mugabe.

Uchaguzi wa kwanza wa rais baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ulifanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 Julai. Katika uchaguzi huo, Rais Emmerson Mnangagwa alishinda kwa asilimia 50.8 ya kura akifuatiwa na mgombea wa chama cha MDC Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura zote.

Kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe kumefuatiwa na wimbi la machafuko na mapigano ambayo hadi sasa yamesha sababisha vifo vya watu sita.../

Tags