Kaimu Rais wa Nigeria alaani kuzuiwa wabunge kuingia bungeni
Hatua ya kuzingirwa Bunge la Taifa la Nigeria jana Jumanne kulikofanywa na askari usalama wa nchi hiyo ambao waliwazuia wabunge kuingia bungeni kwa muda wa karibu saa nzima ilifanywa bila ya ofisi ya Rais kuwa na taarifa. Hayo yamesemwa na Kaimu Rais wa Nigeria ambaye amemfuta kazi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Wanaume kadhaa waliokuwa na silaha waliovalia sare nyeusi kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (DSS) jana walionekana wakiwa wamesimama nje ya milango ya jengo la Bunge la Taifa la Nigeria katika mji mkuu Abuja. Maafisa polisi kadhaa baadaye waliungana na wanaume hao.
Msemaji wa Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbanjo amesema kuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa Musa Daura amefutwa kazi. Makamu wa Rais ndiye anayekaimu kiti cha Rais Muhammad Buhari wa Nigeria ambaye kwa sasa ameenda mapumzikoni nje ya nchi. Osinbanjo amesema kuwa hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria iliyofanywa bila la Ofisi ya Rais kuwa na taarifa inalaaniwa na inapingwa kikamilifu.