Upinzani wazidi kupata pigo Tanzania, Mtatiro naye ahamia CCM + SAUTI
Mrengo wa upinzani nchini Tanzania umeendelea kupata pigo kutokana na viongozi wake mashuhuri kuhamia chama tawala cha Mapinduzi CCM baada ya Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Chama cha CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza leo kwamba, amekihama chama hicho na kuhamia CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari, Julius Mtatiro ametangaza kuwa huu ni wakati wa kwenda kutumia vipaji vyake kikamilifu pia kuwa balozi mkubwa wa Rais Magufuli ndani na nje ya nchi.
Akifafanua zaidi kuhusiana na hatua yake hiyo, kada huyo wa zamani wa Chama cha Wananchi CUF amesema kuwa, ameamua kuchukua uamuzi huo kwa kuwa jukwaa alilokuwa analisimamia katika siasa kwa miaka kumi limeshindwa kumpa nafasi ya kuifanyia nchi yake maendeleo.
Aidha amesema bayana kwamba, ametafakari kwa miaka zaidi ya kumi aliyofanya na kuona kuwa, umefika wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hatua ya kada huyo wa ngazi za juu wa chama cha CUF kuondoka upinzani inakuja siku chache tu baada ya Mwita Waitara aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hamahama hiyo ya wapinzani imekuwa ikielezwa kuwa, inatishia mustakabali wa upinzani nchini Tanzania. Hatua ya wapinzani kuhamia chama tawala CCM inaelezwa na baadhi ya Watanzania kuwa inasababishwa na njaa ya wanasiasa hao, huku kundi la pili likisema kuwa, inatokana na udikteta walionao baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao wamevifanya vyama hivyo kama mali yao.