Algeria yalaani jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Ghaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria amelaani vikali jinai za wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Katika taarifa yake maalumu, Abdul Aziz bin Ali al-Sharif ameelezea mshikamano wa Algiers na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kusisitiza kuwa, Algeria itaendelea kuwaunga mkono wananchi hao hadi watakapopata haki zao zote.
Vile vile ameitaka jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina kama ambavyo amelitaka pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lake la kukomesha jina za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Wapalestina watatu wameuawa shahidi na zaidi ya 80 wengine wamejeruhiwa baada ya wanajeshi makatili wa Israel kuwashambulia wananchi hao waliokuwa wanaandamana kwa amani katika Ijumaa ya 20 ya maandamano ya "Haki ya Kurejea."
Maandamano ya amani ya "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu wa 2018 kwa mnasaba wa maadhimisho ya "Siku ya Ardhi" huko Ukanda wa Ghaza na yamekuwa yakiendelea kila Ijumaa.
Hadi hivi sasa Wapalestina 161 wameshauawa shahidi na zaidi ya 17 elfu wengine wamejeruhiwa katika mashambulizi ya wanajeshi wa Israel wanaojaribu kukandamiza maandamano hayo.
Nchi nyingi duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na taasisi za kimataifa zimekuwa zikilaani mara kwa mara jinai hizo.