NATO, sababu kuu ya mgogoro wa ndani nchini Libya
Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya Khalifa Haftar amesema kuwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) ndiyo sababu ya hali mbaya inayoshuhudiwa sasa nchini humo.
Khalifa Haftar amesema mashambulizi ya NATO yaliharibu kabisa miundombinu ya Libya na kutayarisha uwanja wa kujitokeza makundi ya kigaidi kama al Qaida na Daesh nchini humo na ametahadharisha kwamba, baadhi ya wanasiasa wanataka kuendelea hali ya sasa nchini Libya kwa shabaha ya kulinda maslahi yao.
Matamshi hayo ya Jenerali Haftar yametolewa baada ya kupita yapata miaka 8 sasa tangu majeshi ya nchi za Magharibi chini ya mwavuli wa shirika la NATO yaliposhambulia miji mbalimbali ya Libya. Kwa maana nyingine ni kuwa, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ziliparamia mawimbi ya harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddaf na kuharibu miundombinu na taasisi zote muhimu za nchi hiyo kwa kutumia makombora na ndege za kivita. Japokuwa wakati huo ilidaiwa kuwa, mashambulizi ya NATO nchini Libya yanafanyika kwa lengo eti la kulinda raia wa nchi hiyo lakini ukweli ni kwamba miongoni mwa malengo makuu ni pamoja na kujenga mazingira mapya ya kisiasa katika eneo la kaskazini mwa Afrika na kuanza kuinyonya nchi hiyo.
Kuvunjwavunjwa miundombinu ya Libya, vikwazo vya kijeshi, kuwepo kwa silaha nyingi haramu, harakati za makundi ya kigaidi na waasi na vita vya kuwania utajiri wa Libya baina ya nchi za Magharibi na nyingine za kikanda sasa vimeitumbukiza Libya katika hali ya ukosefu wa amani na umaskini. Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Khemaies Jhinaoui anasema: "Madola makubwa yameifanya Libya kuwa uwanja wa vita vinavyopiganwa kwa niaba yao."
Kuendelea kwa vita hivyo na machafuko ya ndani vimepelekea kuimarika zaidi makundi ya kigaidi nchini humo kiasi kwamba, licha ya kundi la Daesh kupata kipigo cha mbwa koko katika nchi za Iraq na Syria lakini kundi hilo limezidi kujiimarisha nchini Libya. Mtaalamu wa masuala ya Mashariki (Orientalist) na mwanadiplomasia wa zamani wa Russia anasema: "Walibya wanapaswa kufanya haraka kuboresha hali ya usalama nchini humo ili magaidi walioshindwa katika nchi za Syria na Iraq wasikimbilie maficho katika nchi hiyo."
Libya inaendelea kuteseka na athari mbaya za mashambulizi ya majeshi ya NATO kwa miaka 8 sasa huku nchi za Magharibi zikiendelea kulumbana juu ya jinsi ya kugawana keki ya nchji hiyo. Kwa msingi huo zinakwamisha kwa njia moja au nyingine mchakato wa kupatikana amani nchini Libya ili kuweza kuvua samaki katika maji machafu.
Misimamo ya nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu kuhusiana na Libya inafichua malengo yao halisi na yasiyo ya kibinadamu kuhusu nchi hiyo. Katika uwanja huo tunaweza kuashiria juhudi zinazofanywa na baadhi ya nchi za Magharibi za kutaka kuwa na ushawishi nchini Libya na kudhibiti utajiri wa mafuta wa gesi wa nchi hiyo, kudhibiti maeneo ya kistratijia kama bandari za mavuta na kadhalika na kuitumia Libya kama lango la kuingia maeneo ya kaskazini na katikati mwa Afrika.
Katika hali kama hii inaonekana kuwa njia pekee ya kuiokoa Libya ni kufanya mapatano ya kitaifa na baadaye kuitisha uchaguzi huru utakaoyashirikisha makundi yote bila ya kuingiliwa na nchi za kigeni.