Watu wasiopungua 40 wauawa mashariki mwa Ethiopia
Wanamgambo wenye silaha wameua watu wasiopungua 40 mashariki mwa Ethiopia mwishoni mwa wiki katika wimbi la machafuko yaliyochochewa na migawanyiko ya kikabila.
Watu karibu 100 wamekuwa wakimbizi kufuatia machafuko yaliyoathiri eneo la mpaka kati ya Somalia na mikoa ya Oromiya. Negeri Lencho msemaji wa mkuu wa mkoa wa Oromiya amesema kuwa wanamgambo waliokuwa wamejizatiti kwa silaha nyingi kutoka mkoa wa Somalia ndio waliofanya shambulio hilo la kuvuka mpaka katika wilaya ya Hararghe mashariki mwa mkoa wa Oromiya.
Maafisa katika mkoa wa Oromiya wamewatuhumu wanamgambo hao wanaofahamika kwa jina la "vikosi vya Liyu" kuwa mwaka jana walihusika katika mashambulizi kadhaa katika eneo hilo.
Machafuko ya kikabila yalienea katika mkoa wa Oromiya tangu kujiri maandamano mwaka 2015 ya kudai kupatiwa haki ya kumiliki ardhi. Askari usalama waliuawa mamia ya watu katika machafuko ya zaidi ya miaka miwili katika mkoa wa Oromiya.