UN kuchunguza mauaji ya watu 14 eneo la Kuda Sudan Kusini
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umeanza kuchunguza mauaji ya watu 14 waliouawa wakati wa mapigano baina ya jamii za wafugaji nje ya Juba, mji mkuu wa nchi hiyo.
Mapigano hayo yamejiri Kuda, kijiji kilichopo kilometa 72 kusini mwa mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
Maafisa wa UNMISS wametembelea eneo hilo na kubaini kuwepo makaburi mapya kabisa, walikozikwa watu hao 14 waliotokana na mapigano.
Taarifa zinasema wanawake na watoto wamekimbia makazi yao na kupata hifadhi kwenye chumba cha darasa la shule moja ya msingi.
Kumekuwepo ripoti za ghasia kufuatia madai ya kwamba jamii moja ilishambulia nyingine kwa lengo la kuiba misaada ya kibinadamu iliyotolewa na shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula la WFP.
Wakati Sudan Kusini bado inaonekana kuwa ni moja ya maeneo hatari kwa wahudumu wa misaada kufanya kazi zao, walinda amani wa UNMISS wanaendelea na doria iwe ni katika ziara za kutathmini hali ya usalama au ulinzi kwa lengo la kuweka mazingira bora na salama.
Hayo yanajiri wakati ambao Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkubwa, Riek Machar wamehimiza kuheshimiwa kikamilifu mapatano ya mwisho ya kugawana madaraka kwa shabaha ya kukomesha vita vya ndani vya umwagaji mkubwa wa damu vilivyodumu kwa miaka mitano sasa.
Mapatano hayo yalitiwa saini siku chache zilizopita mjini Khartoum, Sudan mbele ya mataifa ya Sudan, Kenya, Uganda na Djibouti.