Mahasimu Sudan Kusini wasisitiza kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani
Pande mbalimbali zinazojihusisha na mchakato wa amani wa Sudan Kusini, zimewasisitizia watu wa nchi hiyo kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani ya Khartoum.
Ahadi hiyo imo kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumanne na Shirika la Maendeleo ya Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD. Pande hizo pia zimeapa kuendelea na juhudi za kutafuta umoja, amani na ustawi katika msingi wa haki, usawa na kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
Taarifa pia imesisitiza kuwa vita na mapambano nchini Sudan Kusini vimesababisha mateso yasiyoelezeka kwa watu wa nchi hiyo, na kuharibu jamii ya nchi hiyo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita pande zinazopambana nchini humo zilisaini Makubaliano ya Amani ya Khartoum nchini Sudan, ukiwemo usitishaji vita wa kudumu ulioanza kutekelezwa ndani ya saa 72.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkubwa, Riek Machar wamehimiza kuheshimiwa kikamilifu mapatano ya mwisho ya kugawana madaraka kwa shabaha ya kukomesha vita vya ndani vya umwagaji mkubwa wa damu vilivyodumu kwa miaka mitano sasa.
Mapatano hayo yalitiwa saini siku chache zilizopita mjini Khartoum, Sudan mbele ya mataifa ya Sudan, Kenya, Uganda na Djibouti.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.