Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini kuanza tena mjini Khartoum
Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yanatarajiwa kuanza tena mjini Khartoum katika nchi jirani ya Sudan Jumatatu ijayo. Mazungumzo hayo yalikuwa yameahirishwa kutokana na sherehe za Idul Adh'ha zilizoanza Jumanne iliyopita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, ambaye pia ni mwenyekiti wa mazungumzo hayo, awali alikuwa amesema mazungumzo hayo yataanza Jumapili. Baadhi ya duru zinasame mkataba rasmi wa amani nchini Sudan Kusini unatarajiwa kutiwa saini. Mkataba huo unahimiza kuachiliwa huru kwa wafungwa, utoaji wa misaada ya kibinadamu na kuundwa serikali ya mpito ndani ya miezi minne.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua kuwa mazungumzo yanayoendelea kwa sasa, yanakwenda vizuri.
Michael Makuei amesema, pande hasimu nchini humo zimefikia mwafaka kuhusu mswada wa mkataba rasmi na wa mwisho wa amani, ambao unatarajiwa kusainiwa Agosti 27, huko Khartoum.

Amesema mazungumzo ya sasa yanahusu masuala ambayo hayajatatuliwa ya kugawana madaraka na mipango ya usalama.
Naye Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nicholas Haysom ametaka pande zote kushughlulikia kikamilifu suala la usalama katika mkataba huo.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkubwa, Riek Machar wamehimiza kuheshimiwa kikamilifu mapatano ya mwisho ya kugawana madaraka kwa shabaha ya kukomesha vita vya ndani vya umwagaji mkubwa wa damu vilivyodumu kwa miaka mitano sasa.
Mapatano hayo yalitiwa saini Agosti 5 mjini Khartoum, Sudan, mbele ya mataifa ya Sudan, Kenya, Uganda na Djibouti.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.