Riek Machar akataa kusaini rasimu ya makubaliano ya amani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47742-riek_machar_akataa_kusaini_rasimu_ya_makubaliano_ya_amani_sudan_kusini
Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, amekataa kutia sahihi rasimu ya hivi karibuni ya mkataba wa amani na serikali ya Juba ambayo ingemaliza mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2018 07:46 UTC
  • Riek Machar akataa kusaini rasimu ya makubaliano ya amani Sudan Kusini

Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, amekataa kutia sahihi rasimu ya hivi karibuni ya mkataba wa amani na serikali ya Juba ambayo ingemaliza mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan, Al-Dirdiri Mohamed. Mohamed ameongeza kuwa, chama cha Riek Machar na kundi jingine vimekataa kutia saini rasimu hiyo vikitaka dhamana kuhusu matakwa yao.

Hatua hiyo ya Riek Machar ya kukataa kutia saini rasimu ya sasa ya makubaliano ya amani nchini Sudan ni ishara ya mashaka na vikwazo vilivyopo katika njia ya utekelezaji wa makubaliano hayo.

Mwezi uliopita Machar na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini walitia saini makubaliano ya kusitisha vita na kugawana madaraka. Makubaliano hayo yanayosimamiwa na Sudan yangali yanakabiliwa na visingiti kadhaa kuhusu namna ya utekelezaji wa baadhi ya vipengee vyake.

Mamilioni ya Wasudan Kusini wamekimbia makazi yao.

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazika kukimbia makazi na hata nchi yao huko Sudan Kusini kutokana na vita vya ndani baina ya jeshi la serikali ya Juba na kundi la waasi linaloongozwa na Riek Machar.