Makundi hasimu Libya yafikia makubaliano ya kusimamisha vita mjini Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47907-makundi_hasimu_libya_yafikia_makubaliano_ya_kusimamisha_vita_mjini_tripoli
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia masuala ya Libya jana jioni ilitangaza habari ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita baina ya makundi yenye silaha mjini Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2018 22:29 UTC
  • Makundi hasimu Libya yafikia makubaliano ya kusimamisha vita mjini Tripoli

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia masuala ya Libya jana jioni ilitangaza habari ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita baina ya makundi yenye silaha mjini Tripoli.

Kamati hiyo imesema kuwa, Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amekutana na wawakilishi wa makundi yanayohusika katika mapigano ya mjini Tripoli na kuyakinaisha yasimamishe mapigano. Kwa mujibu wa kamati hiyo, kikao hicho kimefanyika mjini Zawiya. Juzi Jumatatu, Umoja wa Mataifa uliyataka makundi yote hasimu yashiriki kwenye kikao hicho.

Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya

 

Kabla ya hapo pia, vyombo vya habari vya Libya vilikuwa vimetangaza habari ya kusimamishwa mapigano mjini Tripoli lakini mara zote mapigano hayo huwa yanaanza upya muda mchache baada ya kutangazwa habari za kusimamishwa.

Mji mkuu wa Libya Tripoli umekuwa uwanja wa mapigano baina ya makundi hasimu tangu siku ya Jumapili ya tarehe 26 Agosti. Habari zinasema kuwa watu 61 wameshauawa na 159 wengine wameshajeruhiwa katika mapigano hayo tangu siku hiyo hadi hivi sasa.

Hali si shwari katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

 

Libya ilitumbukia kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kuungasha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Katika uvamizi huo, NATO na Marekani zilishambulia kinyama miundombinu ya Libya na kuivuruga kabisa.

Baada ya hapo ziliitelekeza nchi hiyo ya Kiarabu ya Kaskazini mwa Afrika baada ya kulivunja jeshi lake, na kuacha silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi hasimu ambayo kila moja lilikuwa linataka kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo. Hivyo tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kuwa na utulivu wa angalau siku moja. Mivutano baina ya makundi mbalimbali yanayoungwa mkono na madola ajinabi ni sababu kuu ya kukosekana utulivu huko Libya.