Sudan Kusini yawafunga jela wanajeshi wabakaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47963-sudan_kusini_yawafunga_jela_wanajeshi_wabakaji
Mahakama ya jeshi Sudan Kusini imewahukumu vifungo virefu wanajeshi 10 waliowabaka wafanyakazi wageni watoa misaada, mbali na uporaji na mauaji yaliyotokea upya mwezi Julai 2016.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2018 11:26 UTC
  • Sudan Kusini yawafunga jela wanajeshi wabakaji

Mahakama ya jeshi Sudan Kusini imewahukumu vifungo virefu wanajeshi 10 waliowabaka wafanyakazi wageni watoa misaada, mbali na uporaji na mauaji yaliyotokea upya mwezi Julai 2016.

Mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi ya nchi hiyo, Brigedia Jenerali Neath Almaz Juma, amesema kuwa, baadhi ya wanajeshi watatumikia kifungo cha miaka 10 gerezani,  wengine kifungo cha miaka kati ya 7 na 14 na wengine kifungo cha maisha.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa jeshi, mahakama iliwaalika mashahidi kutoka nchi za nje ili kukamilisha kesi yao iliyoakisiwa sana na vyombo vya habari, na kufuatiliwa na wanadiplomasia, baada ya Idara ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yasio ya kiserikali, kulalamikia ucheleweshaji wa kesi hiyo. Haya yanajiri baada kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini kukubali kutia saini makubaliano ya mwisho ya mkataba wa amani na serikali ya Juba ambayo yatamaliza mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar (kushoto) na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo

Mvutano wa kisiasa nchini Sudan Kusini uliibuka mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kwamba anataka kumpindua. 

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuyakimbia makazi na hata nchi yao huko Sudan Kusini kutokana na vita vya ndani baina ya jeshi la serikali ya Juba na kundi la waasi linaloongozwa na Riek Machar.

Asasi mbalimbali zimekuwa zikitahadharisha kuhusu kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.