Sep 15, 2018 07:42 UTC
  • Shambulio la Boko Haram laua watu 8 kaskazini mashariki mwa Nigeria

Watu wasiopungua wanane wanaripotiwa kuuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kuvishambulia vijiji viwili.

Babakura Kolo, mmoja wa makamanda wa makundi ya wanamgambo yanayoendesha operesheni dhidi ya Boko Haram amesema kuwa, magaidi wa Boko Haram wamefanya mashambulio dhidi ya vijiji viwili kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua watu wanane.

Aidha amesema kuwa, wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram mbali na kufanya mauaji hayo wamepora mali za wanavijiji hao.

Shambulio hilo la Boko Haram linaripotiwa katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni magaidi hao wameshadidisha mashambulio yao dhidi ya ngome za jeshi na makazi ya raia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hivi majuzi pia kundi la kigaidi la Boko Haram lilishambulia kambi nyingine ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo lakini shambulio hilo lilizimwa na wanajeshi wa serikali ya Abuja.

Kundi hilo la kigaidi lilianzishwa mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria na hadi hivi sasa limeshaua zaidi ya watu 20 elfu nchini Nigeria na katika nchi jirani na limeshapelekea zaidi ya watu milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ameendelea kukosolewa kutokana na kutotekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni ambapo moja ya ahadi hizo ilikuuwa ni kulitokomeza kundi la kigaidi la Boko Haram.

Tags