Viongozi wa Eritrea na Ethiopia wasaini makubaliano ya amani, uhusiano wazidi kuimarika
Viongozi wa Ethiopia na Eritrea wametia saini makubaliano ya amani huku uhusiano wa nchi hizo mbili jirani zilizokuwa na uadui mkubwa ukizidi kuimarika siku baada ya siku.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki wametia saini makubaliano hayo mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Vipengee vya makubaliano hayo havijatangazwa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kuwa makubaliano hayo yana vipengee saba, ingawa hata hivyo Eritrea haikutoa maelezo yoyote.
Maafisa wa Saudi Arabia nao wamekataa kujibu maswali waliyoulizwa kuhusu vipengee vya makubaliano hayo.
Wiki iliyopita, viongozi wa nchi hizo mbili walifungua mipaka yao na walisherehekea kwa pamoja Mwaka Mpya wa Ethiopia katika mpaka wao wa pamoja.
Nchi hizo mbili jirani zilikuwa na ugomvi wa muda mrefu huku Ethiopia ikikataa kutekeleza amri ya Umoja wa Mataifa ya kuirejeshea Eritrea ardhi yake iliyoiteka katika vita vya 1998-2000.
Hata hivyo mwezi Juni 2018, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed alitangaza kuwa nchi yake itatekeleza amri ya mwaka 2002 ya Umoja wa Mataifa ya kuondoa wanajeshi wake katika ardhi hiyo ya Eritrea. Mwezi mmoja baadaye nchi hizo mbili zilitiliana saini makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara baina yao na hivyo kumaliza miongo miwili ya uadui na ugomvi kati ya nchi hizo jirani.