Polisi: Watu 23 wameawa katika machafuko ya hivi karibuni nchini Ethiopia
Polisi ya Ethiopia imetangaza kuwa, kwa akali watu 23 wameuawa katika machafuko yaliyoibuka hivi karibuni jirani na mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa.
Ghasia hizo zilianza Jumatano iliyopita baada ya wafuasi wa kundi la zamani la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Oromo (OLF) ambao wengi wao wanatoka kabila la Oromo, kuingia mjini Addis Ababa wakipeperusha bendera ya OLF, na kupambana na wakazi wa mji huo.
Waoromo ambao ni takribani asilimia 33 ya watu wote milioni 100 nchini Ethiopia wanaitazama OLF na bendera yake kuwa ni nembo ya mapambano ya miongo kadhaa ya kupinga ubaguzi wa watawala wasio Waoromo nchini humo.
Hata hivyo Waethiopia wasio Waoromo wanaoitazama OLF na bendera yake kuwa ni nembo ya kutaka kujitenga eneo kubwa la Oromia kutoka Ethiopia.
Polisi ya Ethiopia imesema kuwa, watu wasiopungua 70 wametiwa mbaroni wakihusishwa na machafuko hayo ambayo yamelaaniwa vikali na Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa nchi ambaye tangu aingie madarakani amefanya mabadiliko makubwa hususan ya kuboresha uhusiano wa nchi hiyo na jirani yake Eritrea.
Wakati huo huop wananchi wenye hasira jana (Jumatatu) walifanya maandamano katikati mwa mji mkuu Addis Ababa wakilaani mauaji hayo.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa Ethiopia kutoka jamii ya Oromia, ametahadharisha kuwa, kuna watu wanaotaka kuchochea ghasia kwa kisingizio cha utata wa bendera hiyo.