UN yaeleza wasiwasi wake kuhusu vitendo vya ukatili Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba una wasiwasi kuhusu vitendo vya ukatili na mateso dhidi ya raia hususan wanawake na watoto wadogo vinavyoendelea kufanyika Sudan Kusini.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, ripoti iliyotolewa hivi karibini na Tume ya Haki za Binadamu ya umoja huo kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili unaofanyika Sudan Kusini inatia wasiwasi mkubwa.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, wahanga wa ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini hususan wanawake waliofanyiwa ukatili wa kingono wanapaswa kutendewa uadilifu, kulipwa fidia na kupata huduma za tiba haraka iwezekanavyo.
Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini pia imeashiria mateso na ukatili wa kingono unaofanyika katika nchi hiyo na kusisitiza udharura wa kushughulikiwa uhalifu uliofanyika dhidi ya raia.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya jeshi la serikali ya Rais Salva Kiir na waungaji mkono wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.