Sep 28, 2018 14:35 UTC
  • Kundi la Boko Haram lashambulia kambi ya jeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi la kigaidi la Boko Haram limefanya shambulio jingine dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamefanya shambulio jipya dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, magaidi hao wa Boko Haram wameshambulia kambi ya jeshi ya Gashigar katika eneo la Mobbar katika jimbo la Borno. 

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Nigeria, wanamgambo hao wa Boko Haram walikusudia kupenya na kuingia katika kambi hiyo, lakini vikosi vya serikali vilikuwa macho na hivyo vikasambaratisha njama hiyo.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ambaye serikali yake inakosolewa kwa kushindwa kulitokomeza kundi la kigaidi la Boko Haram

Hadi sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusiana na idadi ya waliouawa katika shambulio hilo iwe ni wanamgambo wa Boko Haram au wanajeshi wa serikali.

Shambulio hilo limekuja siku chache tu baada askari wa jeshi la Nigeria kuwaua magaidi 14 wa kundi la Boko Haram katika operesheni inayolenga kutokomeza mabaki ya kundi hilo la kigaidi katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la eti kuasisi utawala wa Kiislamu katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambapo hadi sasa limeshaua zaidi ya watu elfu ishirini na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.

Tags