Mkosoaji mkubwa wa Rais Kagame wa Rwanda, Diane Rwigara aachiwa huru
Vyombo vya Mahakama nchini Rwanda vimemuachia huru kwa dhamana mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mashuhuri wa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo Diane Rwigara, ingawaje kwa masharti.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Rwanda, Claire Bukuba amesema leo Ijumaa kuwa, Rwigara pamoja na mama yake wameachiwa huru kwa dhamana lakini wametakiwa kutotoka katika mji mkuu Kigali mbali na kukabidhi pasi zao za kusafiria kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali.
Tarehe 30 mwezi Agosti mwaka jana, wawili hao walichukuliwa nyumbani kwao Kigali na maafisa wa polisi kwa madai ya kukwepa kulipa kodi zinazoihusu kampuni ya tumbaku inayomilikiwa na familia yao.
Kabla ya hapo, Diane Shima Rwigara alituhumiwa kughushi na kufanya udanganyifu katika fomu alizojaza kwa ajili ya kugombea urais Agosti mwaka jana akitaka kuchuana na Rais Kagame. Hata hivyo baadaye aliondolewa katika kinyanganyiro hicho kwa kile kilichotajwa kuwa ni kushindwa 'kutimiza masharti'.
Mwanasiasa huyo wa upinzani aliye na umri wa miaka 35 na ambaye ni mhasibu kitaaluma amekuwa akimtuhumu Rais Kagame kwamba anawabinya wapinzani; na kukikosoa chama tawala cha RPF kwa kuweko madarakani tangu kiliposhika hatamu za uongozi baada ya kuhitimisha mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.