Libya yapinga uingiliaji wa kijeshi wa madola ajinabi nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48617-libya_yapinga_uingiliaji_wa_kijeshi_wa_madola_ajinabi_nchini_humo
Mjumbe wa Baraza Kuu la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amepinga njama za jeshi la nchi za Magharibi NATO za kutaka kuingilia tena kijeshi nchini humo na kusema kuwa, Libya inapinga uingiliaji wowote wa kijeshi wa madola ya kigeni.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Oct 06, 2018 15:13 UTC
  • Libya yapinga uingiliaji wa kijeshi wa madola ajinabi nchini humo

Mjumbe wa Baraza Kuu la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amepinga njama za jeshi la nchi za Magharibi NATO za kutaka kuingilia tena kijeshi nchini humo na kusema kuwa, Libya inapinga uingiliaji wowote wa kijeshi wa madola ya kigeni.

Shirika la habari la Sputnik limenukuu Adel Karmouss, mjumbe wa Baraza Kuu la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya akisema kuwa, wananchi wa nchi hiyo kamwe hawatoruhusu uingiliaji wa madola ya kigeni likiwemo jeshi la nchi za Magharibi NATO, nchini mwao.

Amesisitiza kuwa, uingiliaji wa dola lolote lile katika masuala ya ndani ya Libya utapelekea wananchi wa nchi hiyo waungane wote kupambana nalo.

Makundi hasimu yenye silaha yameenea katika kona zote za Libya

 

Vile vile amesema maeneo mengi ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Tripoli yanadhibitiwa na makundi ya wanamgambo badala ya jeshi na hiyo ndiyo sababu iliyoyafanya baadhi ya makundi yaingie tamaa ya kuishabulia Tripoli kwa nia ya kudhibiti Hazina ya Libya.

Siku ya Alkhamisi, Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, alisema mjini Brussels Ubelgiji kwamba jeshi hilo liko tayari kuingia tena kijeshi huko Libya ili kufufua taasisi zake za kiusalama na kijeshi kwa lengo la kurejesha utulivu na amani nchini humo.

Tangu mwaka 2011 hadi hivi sasa, Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja baada ya Marekani na NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hivi sasa kuna makundi ya kila namna yenye silaha nchini humo ambapo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi.