Maulamaa Algeria walalamikia marufuku ya vazi la Burqa makazini
Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu ya nchini Algeria imelalamikia uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kupiga marufuku kuvaliwa na wanwake wa Kiislamu vazi la Burqa katika maeneo ya kazi.
Jumuiya hiyo ya Maulamaa wa Kiislamu ya Algeria ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya kidini nchini leo imetora taarifa ikilalamikia uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku vazi la burqa ofisini na kueleza kuwa wanawake nchini Algeria wanakumbwa na matatizo makubwa wakiwa kazini. Matatizo hayo ni pamoja na udhalilishaji wa kijinsia huku wakisumbuliwa pia na vizuizi na kukosekana usawa kwa kiasi kikubwa. Taarifa hiyo imeongeza kuwa ni vyema serikali ya Algiers iyapatie ufumbuzi matatizo tajwa badala ya kupiga marufuku vazi hilo la burqa.
Kitengo cha Wafanyakazi wa sekta ya umma ya Algeria hivi karibuni kilitoa tangazo chini ya anwani "Jukumu la Wafanyakazi na Mavazi Yao" kwamba ni marufuku kwa wanawake kuwa na vazi la burqa sehemu za kazi. Vazi la burqa lilitajwa katika tangazo hilo kuwa ni moja ya vizuizi vya utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu kwa wanawake.