Nov 14, 2018 14:30 UTC
  • Boko Haram yaua wakulima 16 Borno, kaskazini mwa Nigeria

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeshambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua wakulima wasiopungua 16.

Mashuhuda wamesema mauaji hayo yalifanyika jana Jumanne baada ya wanamgambo wa Boko Haram kuvamia vijiji vya Kazaa na Daraa, yapata kilomita 5 viungani mwa mji wa Monguno.

Kiongozi wa wanamgambo, Ibrahim Liman ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Wenzetu waligundua miili 15 katika mashamba yaliyoko kwenye vijiji vya Kazaa na Daraa hapo jana, na wakulima hao waliuawa na Boko Haram juzi Jumatatu."

Amesema mkulima mwingine aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa shambani katika kijiji cha Gremari, umbali wa kilomita 13 kutoka Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno na kwamba wanaendelea kusaka wakulima wengine 35 waliotoweka baada ya hujuma hiyo ya Boko Haram.

Wakazi wa Borno wakikimbilia usalama wao

Haya yanajiri wiki mbili baada ya wapiganaji wa Boko Haram kuwauwa watu wasiopungua 15 katika shambulio dhidi ya vijiji vya Kofa na Dalori vilivyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza mwishoni mwa mwaka 2015 kuwa Boko Haram limesambaratishwa kwa kiasi kikubwa, lakini kundi hilo lingali lina uwezo wa kufanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, maeneo ya karibu yake na katika maeneo mengi ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.  

Tags