HRW: Misri inawazuilia kusikojulikana makumi ya watetezi wa haki za binadamu
(last modified Sun, 18 Nov 2018 14:27:15 GMT )
Nov 18, 2018 14:27 UTC
  • HRW: Misri inawazuilia kusikojulikana makumi ya watetezi wa haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema vyombo vya usalama nchini Misri vimewatia nguvuni na kuwazuilia kusikojulikana makumi ya watetezi wa haki za binadamu tangu mwezi uliopita wa Oktoba hadi sasa.

Michael Page, Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika amesema leo Jumapili kuwa, aghalabu ya watu waliokamatwa ni wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa serikali, na ameitaka serikali ya Misri kufichua waliko wanaharakati hao.

Amesema shirika hilo limethibitisha kuwa watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati 40 wa kisiasa wamekamatwa tangu mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini baadhi ya vyanzo vya habari vinasema waliokamatwa wanapindukia 80.

Amesema serikali ya Cairo inakiuka haki za msingi za wanaharakati hao, kwa kuwakamata na kuwazuilia kusikojulikana tena bila kuwafunguliwa kesi au hata kupewa wakili, kama inavyoagiza sheria ya nchi.

Maafisa usalama wa Misri wakiendeleza kamatakamata 

Hivi karibuni pia, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilitangaza kuwa mateso yanayofanyika katika jela za Misri ni jinai dhidi ya binadamu na kwamba unyanyasaji na mateso hayo yanayofanywa na askari usalama yanapaswa kukomeshwa.

Kwa mujibu wa takwimu za HRW, tangu mwaka 2014 hadi sasa, Wamisri zaidi ya elfu 60 wametiwa nguvuni na baadhi yao wamefariki dunia kutokana na unyanyasaji na mateso ya askari usalama. 

Tags