Hujuma ya anga ya Marekani yaua 37 nchini Somalia
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) na Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) zimedai kuwa mashambulizi ya anga ya wanajeshi wake yamefanikiwa kuangamiza wanachama 37 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia.
Marekani inadai kuwa imeshirikiana na jeshi la Somalia katika hujuma hiyo iliyolenga maficho ya wanamgambo hao wa kitakfiri ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipigania kuiangusha serikali ya Somalia. Hata hivyo taarifa hiyo haijataja sehemu kulikofanyika hujuma hiyo.
Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya Marekani kudai kuwa limeangamiza wanachama wengine 60 wa al-Shabaab katika shambulizi jingine la anga, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga yanayofanywa na ndege zake zisizo na rubani 'drone' nchini Somalia mnamo Juni 2011, lakini hujuma hizo zimeshindwa kulitokemeza kundi hilo la ukufurushaji.

Hii ni katika hali mbayo, mapema mwezi huu utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi hilo la kigaidi na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.
Katika hatua nyingine, watu watano aghalabu yao wakiwa watoto wadogo wamejeruhiwa katika shambulizi la risasi linalodaiwa kufanywa na wanachama wa al-Shabaab, katika kijiji cha Chakama, eneo la Galana Kulalu, kunti ya Kilifi karibu na mji wa Malindi pwani ya Kenya. Polisi ya Kenya imesema raia mmoja wa Italia ametekwa nyara na wanamgambo hao katika hujuma hiyo ya usiku wa kuamkia leo.