Sudan na Misri zaafiki doria ya pamoja mpakani kukabiliana na ugaidi
Sudan na Misri zimekubaliana kulinda doria ya pamoja katika mpaka kati yao na kuzindua kikosi cha pamoja katika siku za baadaye ili kupambana na ugaidi.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya waziri wa ulinzi wa Sudan Awad Ibn Aouf kukutana na mwenzake wa Misri Mohamed Zaki mjini Khartoum. Mkuu wa Kamandi ya Pamoja ya Jeshi la Sudan Kamal Abdul-Marouf amesema, pande mbili zimekubaliana kuhusu kulinda doria ya pamoja katika mpaka, kuunda mfumo wa mpaka na kuzindua kikosi cha pamoja katika siku za baadaye ili kupambana na ugaidi na uhalifu wa kuvuka mpaka.
Pia amesema mazungumzo kati ya mawaziri hao wawili yamepata mafanikio, huku akiongeza kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kuzindua miradi ya pamoja kupitia kupanua mafunzo ya mawasiliano ya maofisa.
Uhusiano kati ya Misri na Sudan umezorota katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mzozo kuhusu ujenzi wa Bwawa la Renaissance nchini Ethiopia ambalo Misri inalitazama kama tishio kwa mtiririko wa maji katika Mto Nile. Sudan inaunga mkono ujenzi wa bwawa hilo kwa msingi kuwa umeme utakaozalishwa utazisaidia nchi za Afrika na hivyo kupunguza umasikini na kuimarisha ustawi.
Misri na Sudan pia zinazozoania eneo la mpakani la Halayeb ambalo sasa linadhibitiwa na Misri. Mwezi Januari Sudan iliwasilisha lalamiko katika Umoja wa Mataifa ikitaka Misri irejeshe ardhi hiyo.