Nchi za Afrika zasisitiza udharura wa kupambana na ugaidi
Nchi zinazoshiriki mkutano wa kimataifa wa kupambana na ugaidi nchini Algeria zimetangaza kwamba, ushirikiano wa nchi za magharibi mwa Afrika unaweza kuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Washiriki katika mkutano huo wanajadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya kiusalama ya eneo la Sahel na jangwa la Afrika, mchango wa jumuiya na taasisi mbalimbali katika kudhamini fedha kwa makundi ya kigaidi, matatizo na changamoto zinazozikabili nchi za magharibi mwa Afrika kutokana na kurejea magaidi katika nchi hizo.
Mkutano huo unaoongozwa na Algeria na Canada kwa pamoja, unahudhuriwa na wawakilishi wa nchi 30 za Afrika, Asia, Ulaya na Marekani na jumuiya 40 za kikanda na kimataifa. Washiriki wanajadili na kuchunguza njia za kupambana na ugaidi na uhalifu wa kupanga.
Woga na wasiwasi wa kurejea magaidi walioko Syria na Iraq katika nchi za Afrika na Ulaya umewalazimisha viongozi wa nchi hizo washirikiane katika kupambana na magenge hayo.
Mkutano huo wa Pili wa Kimataifa wa Kupambana na Ugaidi ambao zaidi unachunguza njia za kuzisaidia nchi za magharibi mwa Afrika kuhusu jinsi ya kupambana na janga hilo ulianza jana katika mji mkuu wa Algeria, Algiers.