Waalgeria wengi wanapinga safari ya bin Salman nchini mwao
Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na gazeti la al Shuruq la Algeria unaonesha kuwa asilimia 72.5 ya wananchi wa nchi hiyo wanapinga ziara ya Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia nchini mwao.
Hata hivyo, vyombo vya habari vya Algeria vimezinukuu duru rasmi zikisema kuwa, licha ya upinzani huo mkubwa sana wa wananchi, lakini bin Salman ataitembelea nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kwa muda sasa baadhi vya vyama na wanasiasa wakubwa pamoja na vyombo vya habari vya Algeria vimekuwa vikitangaza upinzani wao dhidi ya ziara hiyo ya bin Salman vikisema kuwa mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia ni muuaji wa watoto wadogo nchini Yemen na ni mkandamizaji wa vyombo vya habari na watu wenye fikra huru.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria hivi karibuni ililaani mauaji ya mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi aliyekuwa mpinzani wa utawala wa hivi sasa wa Saudi Arabia na ambaye aliuliwa kikatili katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul Uturuki na hadi hivi sasa viongozi wa Riyadh wanakataa kusema wameupeleka wapi mwili wake.
Ziara ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia huko kaskazini mwa Afrika imekumbwa na upinzani mkubwa wananchi, waandishi wa habari na wahaharakati wa masuala ya kijamii wa nchi za eneo hilo.