Mwanamke Mauritania akataa kumpa mkono Bin Salman kulinda maadili ya Kiislamu + Video
Mwanamke mmoja aliyeshiriki katika kumlaki mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia alipowasili Mauritani alikataa kumpa mkono mtawala huyo ambaye alikuwa amemnyooshea mkono.
Kwa mujibu wa taarifa, Mohammad bin Salman ambaye familia yake inajiarifisha kuwa eti ni wahudumu wa Haram Mbili Tukufu za Kiislamu, alipowasili Nouakchott mji mkuu wa Mauritania jana, alijaribu kumpa mwanamke mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa maafisa wa serikali waliomkaribisha. Lakini mwanamke huyo Muislamu wa Mauritania katika kutekeleza mafundisho ya Kiislamu alikataa kumpa mkono.
Taswira zinamuonyesha mwanamke huyo akiwa ameweka mkono wake kifuani ili amfahamishe Bin Salman kuwa hataki kumpa mkono wake lakini mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia alipuuza na kusisitiza kumpa mwanamke huyo Muislamu mkono. Mwanamke huyo alikataa katakata na hivyo bin Salman akaurejesha mkono akiwa ametahayari.
Jana Jumapili Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Arabia aliwasili katika mji mkuu wa Mauritania huku akilakiwa kwa idadi kubwa ya waandamanaji waliokuwa wanapinga safari yake.
Katika siku za Jumamosi na Jumapili, Wamauritania walimiminika barabarani na kuandamana kupinga safari ya bin Salman katika nchi hiyo.
Muungano wa vyama 10 vya kisiasa Mauritania ulitoa taarifa na kulaani vikali safari ya bin Salman nchini humo. Walisema mrithi huyo wa ufalme wa Saudia anashirikiana na Marekani kwa lengo la kuangamiza malengo ya taifa la Palesitna, kukandamiza uhuru wa maoni na kutoa pigo kwa maslahi ya Waarabu na Waislamu duniani.