Mazoezi ya kijeshi ya nchi nne za Afrika yaanza nchini Misri
Majeshi ya nchi nne za Misri, Nigeria, Sudan na Burkina Faso yameanza kufanya luteka na mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika kambi moja ya kijeshi ya magharibi mwa Misri.
Msemaji wa jeshi la Misri, Kanali Tamer el Refai, amesema katika taarifa yake kwamba maneva hayo ya kijeshi yanafanyika katika kalibu ya ushirikiano wa kijeshi wa Jumuiya ya Nchi za Sahel na Sahra na yalianza jana Jumapili katika kambi ya kijeshi ya Mohammad Najib ya magharibi mwa Misri. Kwa mujibu wa Kanali el Refai, mazoezi hayo ya kijeshi yataendelea hadi Ijumaa wiki hii.
Ameongeza kuwa, lengo la luteka hiyo ni kutoa mafunzo ya mbinu za kupambana na vitisho tofauti vya ugaidi ikiwa ni pamoja na mbinu za kuwakomboa mateka, kuleta ushirikiano baina ya vikosi maalumu vya Afrika, kutoa mafunzo ya kuchukua hatua za haraka katika nyakati za dharura na utekelezaji wa operesheni mbalimbali kwa ushirikiano wa pamoja.
Jumuiya ya Sahel na Sahra iliundwa mwaka 1998 mjini Tripoli Libya kwa kuzishirikisha nchi sita za Afrika yaani Libya, Mali, Niger, Chad, Sudan na Burkina Faso. Hata hivyo baadaye nchi nyingine zailijiunga na jumuiya hiyo ambazo ni Eritrea, Benin, Tunisia, Togo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Djibouti, Ivory Coast, Sierra Leone, Senegali, Somalia, Gambia, Ghana, Guinea Bissau, Liberia, Misri, Morocco na Nigeria.