Kampeni za uchaguzi wa rais Congo DR zasimamishwa mjini Kinshasa
Gavana wa jiji la Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesitisha kampeni za uchaguzi rais mjini humo kabla ya zoezi hilo muhimu lililopangwa kufanyika Jumapili ijayo.
Uamuzi huo uliochukuliwa na Gavana Andre Kimbuta wa jiji la Kinshasa ambaye ni mwanachama wa muungano unaotawala unafuatia ukandamizaji mkubwa uliofanywa na askari usalama dhidi ya wafuasi wa kambi ya upinzani wiki iliyopita ambako watu wasiopungua 7 waliuawa. Hatua hiyo pia inakuja baada ya kuchomwa moto maelfu ya mashine za kupigia kura mjini Kinshasa.
Gavana Andre Kimbuta amesema makundi yenye misimamo mikali yanapanga kufanya vurugu na kuchafua amani kupitia kampeni za uchaguzi. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi.
Jiji la Kinshasa linatambuliwa kuwa ngome kuu ya kambi ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Iwapo utafanyika kwa amani na mafanikio, uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao unasubiriwa kwa muda mrefu utakuwa wa kwanza kuwezesha makabidhiano ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia nchini humo baada ya miongo kadhaa ya tawala za kidikteta, mapinduzi na mapigano ya ndani.
Hata hivyo matokeo ya uchaguzi huo unaofanyika kwa ajili ya kuainisha mtu atakayechukua mikoba ya Rais Joseph Kabila ambaye ameongoza Congo DR kwa kipindi cha miaka 18 bado ni kitendawili kutokana na kampeni za uchaguzi zinazotawaliwa na machafuko na ukandamizaji dhidi ya mikutano ya vyama vya upinzani.
Ripoti zinasema Emmanuel Ramazani Shadary anayeungwa mkono na Rais Kabila anakabiliwa na kibarua kikubwa kutoka kwa wapinzani wake wawili kutoka vyama vya upinzani ambao ni Felix Tshisekedi wa chama kikubwa zaidi cha upinzani na Martin Fayulu, mfanyabiashara na mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya Exxon Mobil.