Kongo yajiandaa kuakhirisha uchaguzi wa Rais wa Jumapili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50316-kongo_yajiandaa_kuakhirisha_uchaguzi_wa_rais_wa_jumapili
Uchaguzi wa Rais ulioakhirishwa kwa muda mrefu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huwenda usifanyike Jumapili ijayo kama ilivyokuwa imepangwa, baada ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kuwaambia wagombea wa kiti cha urais kwamba haikuweza kuandaa zoezi la upigaji kura kama ilivyoainishwa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 21, 2018 04:53 UTC
  • Kongo yajiandaa kuakhirisha uchaguzi wa Rais wa Jumapili

Uchaguzi wa Rais ulioakhirishwa kwa muda mrefu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huwenda usifanyike Jumapili ijayo kama ilivyokuwa imepangwa, baada ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kuwaambia wagombea wa kiti cha urais kwamba haikuweza kuandaa zoezi la upigaji kura kama ilivyoainishwa.

Uchaguzi huo ambao umeakhirishwa mara kadhaa tangu mwaka 2016 ulitazamia kumuainisha mrithi wa Rais Joseph Kabila ambaye anapaswa kuondoka madarakani baada ya kushika hatamu za uongozi kwa miaka 18.

Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Alhamisi iliwaita mkutanoni wagombea wa kiti cha rais baada ya vyombo vya habari kutangaza suala la kuakhirisha uchaguzi huo kutokana na kuwepo matatizo ya vifaa vya kupigia kura ambayo yamewachochea wanafunzi wa vyuo vikuu kuandamana Kinshasa mji mkuu wa nchi hiyo.

Mgombea wa kiti cha urais huko Kongo Theodore Ngoy ambaye alishiriki katika mkutano huo jana aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Corneille Nangaa ametangaza kuwa, tume hiyo kiufundi haiwezi kuendelea kusimamia uchaguzi huo wa Jumapili. Nangaa alitaja moto uliochoma karatasi za kupigia kura wiki iliyopita, kuendelea mlipuko wa homa ya Ebola katika mikoa ya mashariki mwa nchi na ghasia za kikabila zilizoyakumba maeneo ya kaskazi magharibi mwa Kongo kuwa sababu kuu  za kucheleweshwa uchaguzi huo.

Polisi Kongo wakipambana na maandamano ya wanavyuo  

Mgombea mwingine wa kiti cha urais huko Kongo Noel Tshiani ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Mkuu wa Tume  ya Uchaguzi ya nchi hiyo amezungumzia kuhusu kuakhirishwa uchaguzi wa rais katika muda wa kati ya siku saba na 14.