Uchaguzi DRC: Wakazi wa Beni wafanya uchaguzi wa mwigo
Licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI kuakhirisha uchaguzi katika maeneo matatu ya nchi hiyo ya Beni, Butembo na Yumbi kutokana na ugonjwa wa Ebola na mapigano ya kikabila, lakini maelfu ya wakazi wa mji wa Beni hii leo wamepanga foleni na kushiriki uchaguzi wa mwigo, wakiwa na lengo la kuidhihaki tume hiyo.
Uchaguzi katika miji hiyo mitatu umepangwa kufanyika Machi 30 mwakani. Hata hivyo wakazi wa Beni wapatao elfu kumi wamejitokeza na kupiga kura, huku wakisisitiza kuwa serikali inawanyima haki yao ya msingi na ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wanaowataka, kwa kutumia visingizio mbalimbali kikiwemo cha Ebola.
Wakazi hao wa Beni wamesikika wakisema "Kupiga kura ni haki yetu" huku wakilalamikia vikali uamuzi wa CENI wa kuakhirisha uchaguzi katika maeneo hayo. Kijana wa miaka 24, kwa jina Jacob Salamu ameviambia vyombo vya habari kuwa, "Nimesubiri kupiga kura tokeo saa 11 alfajiri. Sisi hatuna Ebola. Kabila ni mbaya zaidi ya Ebola yenyewe."
Huku hayo yakijiri, mgombea wa upinzani anayeonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kwa mujibu wa kura ya maoni ya Congo Research Group, Martin Fayulu, muda mfupi baada ya kupiga kura jijini Kinshasa amesema, "Hii leo tunaadhimisha hatima ya Kabila. Huu ni mwisho wa matatizo ya Wakongamani."
Aidha mvua kubwa ambayo imeshuhudiwa mjini Kinshasa na viunga vyake imeathiri zoezi hilo na kulifanya liende kwa mwendo wa kinyonga.
Wakati huohuo, CENI imesema mshindi wa uchaguzi wa rais atatangazwa tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi ujao wa Januari, 2019. Mbali na kuhitimisha uongozi wa Kabila ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2001, wapiga kura pia wamewachagua wabunge na wawakilishi wa mabunge ya mikoa.