Zoezi la kuhesabu kura katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linaendelea + Sauti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50542-zoezi_la_kuhesabu_kura_katika_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo_linaendelea_sauti
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana Jumapili katika nchi hiyo huku wagombea wakuu wa upinzani Felix Tshisekedi na Martin Fayulu wakilalamikia dosari nyingi wanazodai kwamba zilitokea wakati wa kufanyika uchaguzi huo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 31, 2018 09:59 UTC

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana Jumapili katika nchi hiyo huku wagombea wakuu wa upinzani Felix Tshisekedi na Martin Fayulu wakilalamikia dosari nyingi wanazodai kwamba zilitokea wakati wa kufanyika uchaguzi huo.

Wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea, mrengo wa upinzani na muungano unaotawala kila mmoja umedai kuwa, mgombea wake atashinda kiti cha urais. Vital Kamerhe mkuu wa kampeni wa mgombea wa upinzani Felix Tshiseked amesema kuwa, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa, Tshisekedi na mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu wanaongoza bega kwa bega baada ya asilimia 40 ya kura kuhesabiwa.

Ameongeza kuwa, Emmanuel Ramazani Shadaryy anayeungwa mkono na Rais Joseph Kabila amepata asilimia 13 ya kura tu hadi sasa, ingawa asilimia kubwa ya kura bado haijahesabiwa.

Wagombea wa upinzani Martin Fayulu na Felix Tshisekedi

Uchaguzi ni tukio la nadra nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni Mbelgiji imeshuhudia utawala wa kidikteta, mauaji ya kisiasa, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ikiwa Rais Kabila ambaye amekuweko madarakani tangu kuuawa baba yake Laurent Desire Kabila mwaka 2001 ataondoka madarakani baada ya uchaguzi huo, itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kubadilishana madaraka kwa njia ya amani.

Lakini ikiwa matokeo ya uchaguzi huo yataleta mzozo, hali ya usalama inaweza kuzorota haraka, hususan katika eneo la Mashariki kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako kuna makundi kadhaa ya wanamgambo wanaobeba silaha.

Maelezo zaidi yamo kwenye ripoti ya mwandishi wetu Mossi Mwasi...