Zoezi la kuhesabu kura laendelea DRC
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku huduma ya intaneti na ujumbe mfupi wa simu za mkononi (SMS) zikiwa bado zimekatwa kote nchini humo.
Uchaguzi wa Rais nchini Kongo ulifanyika Jumapili huku baadhi ya mikoa ikigubikwa na ghasia na machafuko.
Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge wa mkoa na kitaifa, yamepangwa kutangazwa Januari 6.
Barnabe Kikaya bin Karubi mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Joseph Kabila wa Kongo amesema kuwa huduma za SMS zilisitishwa ili kudumisha hali ya utulivu nchini baada ya kuanza kuenezwa matokeo ya uwongo katika mitandao ya kijamii.
Taarifa zinasema zoezi la kuhesabu kura limekamilika katika miji kama ya Mbandaka, Bunia na Ituri huku wafuasi wa chama kikuu cha upinzani UDPS wakimtuhumu Gavana wa jimbo la Mbuji Mayi, Ngoy Kasonji kuwa amewatumia vijana kwa kuwapa pesa ili kuvuruga zoezi la kuhesabu kura.
Katika kujibu tuhuma hizo, Gavana Ngoy Kasonji amesema ni vijana wa chama cha UDPS ndio wanaosababisha vurugu.
Wagombea watatu wanaochuana vikali kuwania kiti cha urais ni Ramadhan Shadary wa chama tawala FCC, Martin Fayulu wa Lamuka na Felix Tchisekedi wa UDPS.
Raia milioni 46 walijiandikisha kushiriki uchaguzi huo wa kumrithi Joseph Kabila ambaye anatazamiwa kuacha cheo hicho baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka 18.