Marekani yatumia kisingizio cha uchaguzi wa DRC kutuma askari Gabon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50651-marekani_yatumia_kisingizio_cha_uchaguzi_wa_drc_kutuma_askari_gabon
Rais Donald Trump amesema Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetuma makumi ya askari wa nchi hiyo nchini Gabon, kwa ajili ya eti kuwalinda Wamarekani na ubalozi wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2019 04:20 UTC
  • Marekani yatumia kisingizio cha uchaguzi wa DRC kutuma askari Gabon

Rais Donald Trump amesema Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetuma makumi ya askari wa nchi hiyo nchini Gabon, kwa ajili ya eti kuwalinda Wamarekani na ubalozi wa nchi hiyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.

Katika barua kwa Kongresi ya Marekani jana Ijumaa, Trump amesema wanajeshi 80 wa US waliwasili Gabon Jumatano iliyopita, na watasalia katika eneo hilo hadi pale taharuki na wasiwasi wa kuibuka ghasia za baada ya uchaguzi utakapomalizika.

Amesema Marekani itaongeza wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika iwapo italazimika kufanya hivyo.

Hii ni katika hali ambayo timu za waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimesema uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita nchini Kongo DR ulifanyika vizuri kwa kiasi kikubwa, licha ya kasoro za hapa na pale.

Zoezi la kuhesabu kura nchini Kongo DR

Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI inatazamiwa kutoa matokeo ya muda kesho Jumapili, huku mshindi wa uchaguzi wa rais akitarajiwa kutangazwa rasmi kufikia tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari, 2019.

Marekani ambayo kwa sasa ina zaidi ya askari elfu sita katika nchi kadhaa za Afrika, imekuwa ikitumia visingizio mbalimbali kupanua satua yake ya kijeshi katika bara hilo lenye utajiri mkubwa wa maliasili.