Miaka miwili yapita tangu Boko Haram kuteka wasichana Chibok
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5083-miaka_miwili_yapita_tangu_boko_haram_kuteka_wasichana_chibok
Ni miaka miwili sasa tangu magaidi wakufurishaji wa Boko Haram walipowateka nyara wasichana wa shule ya serikali katika mji wa Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 15, 2016 08:00 UTC
  • Miaka miwili yapita tangu Boko Haram kuteka wasichana Chibok

Ni miaka miwili sasa tangu magaidi wakufurishaji wa Boko Haram walipowateka nyara wasichana wa shule ya serikali katika mji wa Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Itakumbukwa kuwa Aprili mwaka 2014 magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara wasichana 276 kutoka shule yao ya bweni katika mji wa Chibok katika jimbo la Borno ambalo ni ngome ya magaidi hao wa kitakfiri huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tokea wakati huo wasichana 57 walifanikiwa kutoroka lakini wengine 219 wanaminika kuwa mikononi mwa kundi hilo la kigaidi. Mashirika ya kibinadamu nchini Nigeria yamesema kuwa idadi kubwa ya wanawake na wasichana Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo bado wanakumbwa na hatari kubwa.

Mratibu wa kibinadamu nchini Nigeria, Fatma Samoura, amesema wakiwa mikononi mwa Boko Haram, wasichana wa Chibok na wengine wengi wameteseka kwa kulazimishwa kuingia katika kikundi hicho cha kigaidi, ndoa za lazima, utumwa wa kingono na ubakaji, huku wakitumiwa pia kubeba mabomu.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Nigeria, Jean Gou, amesema wanawake na wasichana kati ya 2,000 na 7,000 wametekwa, wakiishi katika utumwa wa kingono.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya watoto walioo katika vita, Leila Zerrougui, amesema."Tukumbuke kwamba hii ndiyo hatima ya watoto wa Nigeria, iliyokuwepo hata kabla. Kilichofanyika kwa wasichana wa Chibok kilikuwa tukio tu lililouwezesha ulimwengu kujua kinachofanyika Nigeria."

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.