Misri kuanzisha kivuko cha kibiashara kati yake na Ghaza
Mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametangaza habari ya kuanzishwa kivuko cha kibiashara katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na Misri.
Mahmoud az Zahar amesema kuwa Ghaza haitamhitajia adui Mzayuni iwapo kivuko hicho cha mpakani kitaanzishwa. Al Zahar aliashiria suala la kuanzishwa uhusiano kati ya baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa nchi ambazo zinafanya jitihada za kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni lengo lao ni kulinda tawala zao.
Mbunge huyo wa Bunge la Palestina ameongeza kuwa, nchi za Kiarabu zinapasa kuanzisha ajenda moja ya Kiarabu kwa ajili ya kuwafukuza maghasibu Wazayuni katika ardhi ya Palestina badala ya kuanzisha uhusiano na Israel.
Utawala wa Kizayuni umeligeuza eneo la Ghaza kuwa jela kubwa zaidi duniani kutokana na kulizingira kila upande. Israel ilizidisha mzingiro wake huo Ghaza mwaka 2007 ikazuia kuingizwa suhula na bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama nishati na bidhaa muhimu za mahitajii kwa ajili ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda Ghaza.